Leviticus 8

Kuwekwa Wakfu Kwa Haruni Na Wanawe

(Kutoka 29:1-37)

1 Bwana akamwambia Musa, 2 a“Waletee Haruni na wanawe mavazi yao, mafuta ya upako, fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume wawili na kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu. 3 bKisha kusanya mkutano wote kwenye ingilio la Hema la Kukutania.” 4Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza, na mkutano ukakusanyika kwenye ingilio la Hema la Kukutania.

5Musa akaliambia kusanyiko, “Hili ndilo Bwana ameagiza lifanyike.” 6 cKisha Musa akamleta Haruni na wanawe mbele, akawaosha kwa maji. 7 dAkamvika Haruni koti, akamfunga mshipi, akamvika joho na kumvalisha kisibau. Pia akafunga kisibau juu yake na kukifunga kiunoni mwake kwa mshipi wake uliosokotwa kwa ustadi. 8 eAkaweka kifuko cha kifuani juu yake, na kuweka Urimu na Thumimu
Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.
kwenye hicho kifuko.
9 gKisha akamvika Haruni kilemba kichwani pake, akaweka lile bamba la dhahabu, yaani ile taji takatifu, upande wa mbele wa kilemba, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

10 hNdipo Musa akachukua mafuta ya upako na kuipaka maskani na kila kitu kilichokuwamo ndani yake, kisha akaviweka wakfu. 11 iAkanyunyiza baadhi ya mafuta juu ya madhabahu mara saba, akaipaka madhabahu mafuta na vyombo vyake vyote pamoja na sinia na kinara chake, ili kuviweka wakfu. 12 jAkamimina sehemu ya hayo mafuta ya upako kichwani mwa Haruni, akamtia mafuta ili kumweka wakfu. 13Kisha akawaleta wana wa Haruni mbele, akawavika makoti, akawafunga mishipi na kuwavika vilemba, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

14 kKisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 15 lMusa akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kutakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Kwa hiyo akayaweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu. 16 mPia Musa akachukua mafuta yote yanayozunguka sehemu za ndani, mafuta yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, akayateketeza juu ya madhabahu. 17Lakini fahali, ikiwa pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo, akaiteketeza nje ya kambi, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

18 nKisha Musa akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 19Ndipo Musa akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za madhabahu. 20Musa akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta. 21Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji, na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

22Kisha akaleta kondoo dume mwingine, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, naye Haruni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 23 oMusa akamchinja yule kondoo dume, akaichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Haruni, na juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 24 pPia Musa akawaleta hao wana wa Haruni mbele, akaipaka sehemu ya hiyo damu kwenye ncha za masikio yao ya kuume, juu ya vidole gumba vya mikono yao ya kuume, na juu ya vidole vikubwa vya miguu yao ya kuume. Kisha akanyunyiza damu pande zote za madhabahu. 25 qAkachukua mafuta ya mnyama, mafuta ya mkia, mafuta yote yanayozunguka sehemu za ndani, mafuta yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, na paja la kulia. 26 rKisha kutoka kwenye kikapu cha mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichokuwa mbele za Bwana, akachukua andazi moja, na jingine lililotengenezwa kwa mafuta, na mkate mwembamba; akaviweka hivi vyote juu ya mafungu ya mafuta ya mnyama, na juu ya lile paja la kulia. 27 sAkaviweka hivi vyote mikononi mwa Haruni na wanawe, na kuviinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa. 28 tKisha Musa akavichukua kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kuwa sadaka ya kuwekwa wakfu, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto. 29 uKisha akachukua kidari, kilicho fungu la Musa la kondoo dume kwa ajili ya kuwekwa wakfu, na kukiinua mbele za Bwana kama sadaka ya kuinuliwa, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

30 vKisha Musa akachukua sehemu ya mafuta ya upako, na sehemu ya damu kutoka kwenye madhabahu, na kuvinyunyiza juu ya Haruni na mavazi yake, na juu ya wanawe na mavazi yao. Kwa hiyo akamweka Haruni na mavazi yake wakfu, pamoja na wanawe na mavazi yao.

31 wKisha Musa akamwambia Haruni na wanawe, “Pika hiyo nyama kwenye ingilio la Hema la Kukutania, na uile hapo pamoja na mkate kutoka kwenye kikapu cha sadaka ya kuweka wakfu, kama nilivyoagiza, nikisema, ‘Haruni na wanawe wataila.’ 32Kisha teketeza nyama na mikate iliyobaki. 33 xMsitoke kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa muda wa siku saba, mpaka siku zenu za kuwekwa wakfu ziwe zimetimia, kwa kuwa muda wenu wa kuwekwa wakfu utakuwa siku saba. 34 yLile lililofanyika leo liliagizwa na Bwana ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 35Lazima mkae kwenye ingilio la Hema la Kukutania usiku na mchana kwa siku saba, na kufanya lile Bwana analolitaka, ili kwamba msife; kwa kuwa hilo ndilo nililoamriwa.” 36Kwa hiyo Haruni na wanawe wakafanya kila kitu Bwana alichoamuru kupitia kwa Musa.
Copyright information for SwhKC